Tusimame Kidete Dhidi Ya Uonevu Unaotukabili

بسم الله الرحمن الرحيم

Tangu kuasisiwa sheria ya kishenzi, thakili na ya kibaguzi ya kupambana na Uislamu na Waislamu (ugaidi) kumekuwa   na mauaji, mateso, kamatakamata na idhilali isiyokwisha kwa Waislamu . Na kuna idadi kubwa ya kesi za kubambikiziwa zinazowakabili masheikh, maustadh, walimu na Waislamu wa kawaida. Dhulma hizi zinaongezeka huku miaka ikisonga mbele.

Uadui dhidi ya Uislamu na Waislamu umefikia katika kiwango cha kutisha  na kisichomithilika kitaifa na kimataifa ukiongozwa na Marekani na kuziburuza nchi  changa  kwa hongo inayoitwa misaada ya kupambana na ugaidi.  Katika uadui huu kando na mengi ya dhahiri pia kuna mengi ya siri yanayofanywa kwa kiburi na jeuri dhidi ya Waislamu  kana kwamba wao na dini yao hawana haki katika ulimwengu huu.

            Vita hii inaendelea kuangamiza kila chetu kuanzia roho, viwiliwili, taasisi, vizazi, heshima, mali na kupachikizwa majina mengi mabaya kutokana na imani yetu. Na kila siku tuhuma za mshikemshike zinaongezeka bila ya hata kesi moja kumalizika kwa kutiwa hatiani. Huku wanasiasa nao wakipishana katika kauli zao za udanganyifu juu ya qadhia hizi. Kauli  za hatari na zenye nia mbaya kwa Umma wetu.

Aidha, vita hii dhidi ya Uislamu na Waislamu ni endelevu, kwa kuwa nchi zetu zinajipendekeza kwa mataifa makubwa hususan Marekani ili  kujipatia hongo la fedha kwa gharama ya Waislamu na dini yao. Basi nchi changa hubuni kila aina ya matukio ili kuhalallisha dhulma hizi. Hapa Tanzania kuna matukio mengi kama ya Amboni, Mwanza, milima ya Makolionga Mtwara nk. Yote haya yamebakisha maswala mengi kuliko majibu.

            Katika hali ya kushtadi kwa dhulma tunapenda kuwakumbusha Waislamu na wapenda haki kwa jumla juu ya mambo mawili makubwa:

Kwanza: dhulma yoyote iwe iwavyo ina mwisho. Kwa kuwa hata Firaun licha ya mabavu, kibri, jeuri na mateso yake kiasi cha kufikia kujiita Mungu, mwisho alianguka kifudufudi na kuangamizwa na kaumu yake na kupata nguvu waliokuwa wakidhulumiwa. Allah Taala anasema:

وَنُرِيدُ أَنْ نَمُنَّ عَلَى الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا فِي الأَرْضِ وَنَجْعَلَهُمْ أَئِمَّةً وَنَجْعَلَهُمُ الْوَارِثِينَ (القصص: 5).

Na tunataka kuwafanyia ihsani wanaokandamizwa katika nchi, na kuwafanya wao wawe viongozi, na kuwafanya wao wawe warithi” ( Al-Qasas : 5)

Pili: Licha ya nguvu na ukubwa wa dhulma, dalili za kiakili na kidini zinatufundisha sio kuridhika na hali ya dhulma, bali tunawajibishwa kusimama kidete kupambana dhidi ya dhulma. Ikiwa Allah Taala kakemea sana katika kitabu cha Quran dhidi ya dhulma na madhalimu, na akaleta Mitume AS kupambana na dhulma hizo. Kwa mfano, Nabii Mussa As. alipambana na dhulma za Firaun za kuwakandamiza Bani Israil, Nabii Shuab As alikabiliana na dhulma za vipimo na Mtume Muhammad SAAW ambaye ni Mtume wa mwisho alisimama kupambana nazo kwa kifkra kabla ya dola na kwa nguvu aliposimamisha dola ya Kiislamu. Haya yote ni fundisho kubwa kwetu kusimama imara dhidi ya dhulma na uonevu walau katika hali ambayo Ummah wetu hauna nguvu wala mamlaka kwa kupaza sauti zetu kukemea na kuonesha kutoiridhika na hali hiyo.

Hivyo, ni wajibu kwa sisi Waislamu katika hali ya sasa kujifunga na jukumu la kukemea, kukosoa na kupaza sauti zetu juu dhidi ya dhulma na uonevu unaotukabili kwa mbinu mbalimbali kupitia njia ya kifikra bila ya kutumia nguvu wala mabavu.

Risala ya Wiki No. 80

15 Dhu al-Qi’dah 1441 / 06 Julai 2020 Miladi

https://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir

#KomeshaUkandamizajiWaKisheriaNaUtekaji
#StopOppressiveLawsAndAbduction

Maoni hayajaruhusiwa.