Ujumbe Kutoka Vita vya Banu Qaynukaa (Shawwal 2AH)

0

Ndani ya mwezi kama huu wa Shawwal (Mfunguo Mosi) vita dhidi ya kabila la kiyahudi la Banu Qaynukaa vilitokea kukabiliana na vitimbwi mbalimbali vya mayahudi. Waislamu waliongozwa katika vita hivi na Mtume (SAAW) mwenyewe.

Kabla ya kulielezea tukio lenyewe hapana budi kufahamu ni vitimbi gani mayahudi walivyomfanyia Mtume (SAAW) na Waislamu. Mtume (SAAW) akiwa kiongozi wa dola ya Kiislamu ya Madina, alifunga mikataba na mayahudi waishio Madina na pembezoni mwake.

Mikataba hiyo iliwahakikishia mayahudi usalama wao na dini yao kwa sharti ya kutofanya uadui au kuwa na mafungamano na maadui wa Waislamu hasa maqureishi. Vile vile kumkubali Mtume (SAAW) kama msimamizi na muamuzi wa mwisho juu ya masuala yote baina yao.

Mayahudi licha ya mikataba hii, walitafuta kila fursa ya kusambaratisha nguvu ya Waislamu na dola yao. Kwa mfano, pale aliponyanyuka Yahudi mmoja na kuingia katika baraza waliokusanyika Answar (waliompa nusra Mtume SAAW) na kuanza kuwachochea kwa kuwakumbusha uadui uliokuwepo baina yao kabla ya Uislamu hasa baina ya kabila la Aws na Khazraj. Kwa bahati mbaya Answar waliyasikiliza maneno yake na kuanza kuzozana baina yao hadi kufikia kuahidiana katika uwanja wa kivita!. Mtume (SAAW) kupata taarifa ya tukio hili kwa haraka aliwajia Answar na kuwazindua ubaya wa fitna hiyo, hali ambayo iliwafanya Answar kuangua vilio na kukumbatiana baina yao kwa majuto ya fitna hiyo.

Kutokana na kushamiri kwa vitimbi hivi, Mtume (SAAW) baada ya Vita vya Badri (2 A.H) aliwakusanya mayahudi wa Banu Qaynukaa ndani ya soko lao na kuwatahadharisha matokeo ya vitimbi vyao, na kuwapa mfano wa yaliyowasibu Maqureishi katika Vita vya Badri. Kama vile kuuwawa viongozi wao na kuchukuliwa mateka watu wao. Hadhari hii waliibeza mayahudi na kuendelea na vitimbi vyao.

Siku moja mwanamke wa Kiislamu alikwenda katika soko la Banu Qaynukaa na kuingia duka moja la Sonara wa Kiyahudi. Dukani hapo walimtaka afunue uso wake nae akakataa, hapo wakaifunga nguo yake kwa nyuma bila mwenyewe kujua, aliponyanyuka nguo yake ikafunuka, mwanamke huyo akapiga kelele, na Muislamu aliekuwepo eneo lile akatoa msaada kwa kumuwa yahudi aliyemdhalilisha mwanamke huyo. Tahamaki mayahudi wakashirikiana na kumuua Muislamu huyo.

Mtume (SAAW) baada ya taarifa hiyo alitoka na jeshi lililoelekea moja kwa moja katika viunga vya kabia hilo. Mayahudi hao wakajificha ndani ya ngome yao kwa kumuogopa Mtume (SAAW) na jeshi lake. Mtume aliwazingira kwa muda wa siku 15 na matokeo yake walijisalimisha, na wakaamrishwa wote watoke Madina.
Mtume (SAAW) alizigawa mali zao kwa jeshi lake baada ya kuchukua khumus/ moja katika tano ya ngawira hiyo. Mayahudi wa Banu Qaynukaa walielekea Shamu lakini wengi wao walifariki kutokana na hali mbaya ya waliokuwa nayo.

Ujumbe tunaopata katika vita hivi ni namna gani Mtume (SAW) alivyovizima vitimbi vya makafiri hususani mayahudi dhidi ya Uislamu na Waislamu, kiasi cha kutumia nguvu ya dola kwa kukashifiwa mwanamke mmoja tu wa Kiislamu.
Hali ya Umma wa Kiislamu wakati huu ni mbaya sana. Wanawake wa Kiislamu hunajisiwa kila dakika, huvunjiwa heshma zao, hudhalilishwa hadi kuuwawa na hakuna wa kuwanusuru.

Ni lazima kuwalingania wenye nguvu katika biladi kubwa za Kiislamu, kuunusuru Uislamu na Waislamu kwa kusimamisha Dola ya Kiislamu (Khilafah Rashida ya Pili) itakayokabiliana na kila uadui dhidi ya Uislamu kwa kulinda heshima, ardhi, mali na matukufu yote ya Uislamu na Wislamu

#UislamNiHadharaMbadala

Leave A Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.