Utalii Kamwe Hauwezi Kuiokoa Tanzania Wala Nchi Nyingine Zinazoendelea

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari:
Mnamo tarehe 08/05/2022 Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alizindua filamu ya kitalii ya ‘Royal Tour’ jijini Dar es salaam, baada ya uzinduzi wa awali uliofanyika New York 18/04/2022, Los Angeles 21/04/2022, Arusha 28/04/2022 na Zanzibar 07/05/2022.
Maoni:
Taarifa rasmi kutoka serikali ya Tanzania inasema kuwa filamu hiyo itapelekea uwekezaji katika sekta ya utalii unaotarajiwa kufikia dolari bilioni 5.04 sawa na takribani Tsh trilioni 12 na kuzalisha ajira takribani 300,000 katika mchakato huo.
Ni jambo lisiloingia akilini kufikiria kuwa filamu hiyo itapelekea kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa udhati wake ambao umefikia 9.30% mwaka 2022 na serikali haijatoa ajira kwa miaka saba sasa.
Kwa mujibu wa taarifa za Benki ya Dunia, ni watu 800,000 tu ndio huingia katika soko la ajira kila mwaka. Pia kwa bahati mbaya sana mashirika mengi binafsi yalianza kupunguza wafanyakazi tangu mwaka 2015. Hivyo, ajira 300,000 zinazosemwa zitazalishwa ni kama tone dogo la maji katika bahari.
Filamu hii ilitengenezwa kwa fedha kutoka kwa wanachama wa Baraza la Taifa la Biashara ambalo linajumuisha wanachama kutoka sekta ya ummah na sekta binafsi, ndani na nje ya sekta ya utalii. Fedha zinazofika Tsh bilioni 7 ambazo Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali hawezi kuziingilia matumizi yake. Maswali yanaibuka hapa; Je huu ni mradi wa ummah? Ikiwa ni hivyo, kwanini haukutumia pesa kutoka katika bajeti ya serikali kuu? Jibu la wazi hapa ni kuwa mradi huu ni wa kibinafsi ambao hatima yake utawanufaisha wadhamini waliochangia utengenezwaji wa filamu hiyo na si ummah kiujumla kama inavyodaiwa.
Pia ni jambo la kuhuzunisha kuwa vivutio vingi vya utalii kama mbuga za wanyama, hifadhi za taifa, haziwanufaishi wananchi jumla kiasi cha kufikia baadhi ya watu kuuawa na askari wa serikali wa kulinda hifadhi hizo au kuhamishwa wakaazi wake kutoka makazi yao kwa kisingizio cha kulinda vivutio hivyo. Serikali hiyo hiyo sasa inashughulishwa na kuwaalika mabepari wamagharibi kuja kunyonya rasilimali hizi kwa jina la uwekezaji.
Katika hafla ya uzinduzi wa filamu hiyo nchini Amerika, serikali ilisaini nyaraka za mawafikiano, matangazo, makubaliano ya uwekezaji na mahusiano ya biashara kati ya makampuni ya Amerika na Tanzania. Pia kulikuwa na matangazo kuhusu makampuni ya Amerika yenye mipango ya kujihusisha na uwekezaji nchini Tanzania miongoni mwao ni Astra Energy, Crane Currency na Parallel Wireless.
Nchi zinazoendelea hujaribu kuonesha upande mmoja wa manufaa ya utalii na kuacha kuonesha madhara yake. Nchini Tanzania kwa mujibu wa UNICEF-Tanzania, utalii wa kimagharibi umepelekea madhara mengi ya kijamii na kiutamaduni miongoni mwao ni kuvurugwa kwa utamaduni, ulevi, ukahaba, matumizi ya madawa ya kulevya na masuala yanayohusiana na mmomonyoko wa maadili (The Impact of tourism on communities and children in Zanzibar, UNICEF-Tanzania 2018). Kimsingi madhara ni makubwa kuliko hata haya yaliyotajwa hapa.
Utalii chini ya ubepari mara nyingi unatumika na watendaji wa serikali kufanya ubadhirifu wa fedha na milki za ummah, hutumika kama chombo cha unyonyaji wa wamagharibi kwa nchi zinazoendelea, njia ya kusambaratisha jamii, mmomonyoko wa maadili, starehe za kidunia ili kupumbaza watu na kuwasahaulisha na malengo ya maisha, na zaidi kuwahadaa ili wasione maovu na dhiki zinazosababishwa na mfumo wa ubepari.
Uislamu chini ya dola ya Khilafah Rashidah itaruhusu utalii bila ya kubinafsisha mali za Ummah, kuvuruga fedha za Ummah na bila ya kuwanyanyasa watu wanaoishi karibu na vivutio vya utalii.
Hatua zote za sheria ya Kiislamu zitachukuliwa kuepusha maovu katika jamii na mmomonyoko wa maadili, hali itakayoubakisha utalii kuwa burudani halali inayosukuma katika kuuzingatia uumbaji wa Allah Taala
أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الأَرْضِ فَتَكُونَ لَهُمْ قُلُوبٌ يَعْقِلُونَ بِهَا أَوْ آذَانٌ يَسْمَعُونَ بِهَا فَإِنَّهَا لاَ تَعْمَى الأَبْصَارُ وَلَكِنْ تَعْمَى الْقُلُوبُ الَّتِي فِي الصُّدُورِ (الحج: 46).
“Je hawatembei katika ardhi ili wapate nyoyo(akili) za kufahamia, au masikio ya kusikia? Kwa hakika macho yao hayapofoki, lakini nyoyo zao ndizo ambazo zinazopofuka (TMQ 22:46)
Imeandikwa na Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania
Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Maoni hayajaruhusiwa.