Uzawa wa Mtume (Saaw) Bishara ya Ushindi Kwa Umma Wetu

Amesema Mtume SAAW :

“Mimi ni dua ya baba yangu Ibrahim, ni bishara ya Issa, na mama yangu aliona ndotoni akitoka nuru (tumboni alipokuwa mjamzito) kuyaangazia maqasri ya Sham”. (Imam Ahmad)

Kipenzi chetu Mtume SAAW ni dua ya Ibrahim As. kama Quran inavyotukumbusha:

: رَبَّنَا وَابْعَثْ فِيهِمْ رَسُولاً مِنْهُمْ ْ (البقرة:
“Ewe Mola wetu! Waletee Mtume anaetokana na wao”  (TMQ 2:129)

Na pia ni bishara ya Issa As. alipowaeleza wana wa Israil kama ilivyotajwa ndani Quran:

وَمُبَشِّرًا بِرَسُولٍ يَأْتِي مِنْ بَعْدِي اسْمُهُ أَحْمَدُ (الصف: 6)

”Na mimi ni Mwenye kuwabashiria Mtume baada yangu, jina lake ni Ahmad”. (TMQ 61:6)

Amma kutoka nuru tumboni ni ndoto aliyoiona mama yake SAAW alipokuwa mja mzito akiwa na mimba ya Kipenzi chetu SAAW. Nayo ni bishara ya ushindi unaoendelea wa umma wake mpaka siku ya kiyama. Licha ya umma wake kusibiwa na kufikjwa na mitihani na kutetereka hapa na pale kama hali tuliyonayo leo tangu kuangushwa Khilafah. Ikifafanua bishara hii ya ushindi Tafsiri ya Muhtaswar Ibn Kathir inanena haya:

‘ Na kuhusishwa Sham katika bishara hii ni kutokana na ukweli kwamba Sham itakuwa ndio Makao makuu ya Uislamu katika zama za mwisho (akheri zaman).

Kama alivyosema Mtume SAAW :

”Halitoacha kundi katika Umma wangu kusimama juu ya haki, halitodhurika kwa atakaelipinga , wala halitodhoofika kwa kuwachwa mkono mpaka ije amri ya Mungu(ushindi) Nalo litatoka Shaam” (Bukhar na Muslim)
(Mukhtaswar Ibn Kathir vol. 1 aya 129 Surat Baqara).

Na Sham ni maeneo ya Syria, Lebanon, Palestina, Jordan, na baadhi ya maeneo ya Iraq. Bishara hii ni moja katika nyingi juu ya ushindi wa Umma huu, kama vile pia alivyosema: “Hakika Allah amenisogezea dunia yote nikaona kutoka mashariki mpaka magharibi .Na kwa hakika utawala wa Umma wangu utafika sehemu zote nilizosogezewa. Na nimepewa khazina mbili, nyekundu na manjano”. (Muslim)

Aidha, kuna bishara ya kurudi tena khilfah, baada ya watawala waovu inayosema: ‘kisha itarudi tena Khilafah kwa manhaj ya Utume… au alipobashiri SAAW kuifungua/fathi Constatinopole iliyofunguliwa na Muhammad Fathi, na kufunguliwa kwa Rome ambayo bado haijafunguliwa, lakini ufunguzi wake hauna shaka insha-Allah.

Bishara hizi ni ushindi kwa Umma huu, lakini ni lazima tuweke ufahamu wa kina juu ya dhana na makusudio ya bishara. Kwa kuwa makafiri na masheikh wa vibaraka huleta ufahamu wa kimakosa kiasi cha kuwachanganya hata wenye ikhlasi.

Awali, bishara huingia katika mambo ya kiimani /kiakida, nako ni kuamini mambo ya ghaib ambayo Muislamu huwajibika kuamini kama yalivyo, bila ya kutoa vigezo vya kiakili wala kutizama mawafikiano ya bishara hiyo na mazingira yaliyomzunguuka.

Pili, kuamini bishara maana yake sio kujipweteka na kusubiri bishara hiyo ijiri, na kuacha kufanya kazi ya ulinganizi wa kurejesha dola, au kusema kama wanavyosema baadhi ya makundi kwamba hakuna haja ya kushughulika ‘Khilafah ni ahadi ya Allah Taala’. Hapana shaka ni ahadi ya Allah Taala hakuna anayelipinga hilo, lakini sheria imetufunga kufanya matendo maalum kuiendea bishara hiyo, na kufanya matendo hayo au kutofanya, hakuzuii bishara husika kujiri. Lakini lau hatukufanya matendo tuliyoamrishwa katika mzunguuko wetu wa kibinaadamu tutakuwa na dhambi, kwa kuwa sheria imetutaka tufanye matendo hayo.Hakuna mbora wa kufahamu bishara ya ushindi kama kipenzi chetu Mtume SAAW, lakini alihangaika kutafuta nusra kwa makabila mbalimbali ili asimamishe dola, alihajir Makka kwa siri, alijificha, kukodi mjuzi wa njia, alipigana jihadi nyingi nk. Yote haya si kwa sababu alikuwa na shaka juu ya ushindi alioahidiwa, bali matendo haya huingia katika upande wa amri za Allah Taala ambazo aliwajibika atende na sio kujipweteka kusubiri ushindi. Au masahaba, nao walielewa vyema kuhusu bishara na hawakuwa na shaka juu ya bishara mbali mbali, lakini walifanya matendo waliyotakikana na sheria kuyatenda.

Tatu, bishara tulizopewa lazima zitulize nyoyo zetu Waislamu na sio kutapatapa na kujiingiza katika aibu, fedheha na mitego ya makafiri, kana kwamba hatuna mfumo kamili wa maisha wenye manhaj/njia yake yenye kujitosheleza. Kiasi cha baadhi kudiriki hata kudandia ukafiri kama kuunga mkono vyama vya kikafiri vya kidemokrasia na mchakato wa katiba zao za kikafiri za kiilmania/kisekula na za kitwaghuti. Huku ni kutumiwa kutetea ukafiri kwa kuuvisha guo la Uislamu na kutojiamini na Uislamu ambao bishara ya ushindi iko upande wake.

Mtume SAAW hata katika hali ngumu ya kuteswa watu wake na kunyanyaswa hakujiingiza kuunga mkono tawala za kikafiri wala taratibu/nidhamu zao. Na kwa hakika yeye alipewa kubwa tena kubwa zaidi, na sio kutoa maoni katika katiba ambayo wenye nidhamu yao wakitaka watayachukua maoni hayo na wasipotaka watayatupilia mbali! Bali Mtume SAAW alitaka kupewa ufalme kamwe, na alikataa kata kata. Au pia alipoona masharti ya baadhi ya makabila yaliyotaka kumpa nusra ya kusimamisha dola yanapingana na Uislamu kama vile kabila Amr bin S’asah walipotaka kumpa utawala uwe katika mikono ya kabila hilo. Mtume SAAW alikataa kata kata. Au pale kabila la Bani Shayban nao walipompa masharti ya kuwa wampe Mtume hatamu za madaraka lakini kwa sharti asipigane vita na mafursi, kwa kuwa kabila hilo lina mkataba na Mafursi juu ya jambo hilo. Mtume SAAW alilikataa. Aliyakataa masharti haya yote na akasimama na msimamo wa thabiti wa Kiislamu wala hakuleta kisingizio cha maslahi ya Waislamu. Licha ya kujua kwa yakini kwamba watu wake wanateswa, wana tabu, mashaka kiasi cha kuwa hali mbaya ya kuhitaji nusra ili wapate faraja.

Ajabu ni kwamba hatuzingatii kwamba makafiri hawaongozwi na wahyi, wala hawana bishara yoyote upande wao, bali wanaongozwa na matamanio yao na mipango ya akili zao finyu. Lakini hujiamini katika kusukuma ajenda zao za kipotofu na huzileta kwa Wislamu moja kwa moja (radically) bila ya kusitasita wala kupinda panda. Basi iweje sisi Waislamu ambao Allah Taala yuko upande wetu , bishara za kipenzi chetu SAAW ziko upande wetu na tunafuata dini ya haki, tujiingize katika fedheha na udhalilifu kwa kunyenyekea katika mfumo wao batil?

Ni wajibu wetu Waislamu katika kipindi hiki cha Mfunguo Sita tunachokumbuka uzawa wa kipenzi chetu SAAW, kurejea juu ya mstari wetu wa ulinganizi wa kurejesha maisha ya Kiislamu kwa kupitia kusimamisha Khilafah katika nchi kubwa za Waislamu, kwa kutumia manhaj aliyotuonesha Mtume SAAW ya mgongano wa kifikra na mapambano ya kisiasa bila ya kuhusisha nguvu, mabavu wala silaha.

#MuhammadNuruYetuKigezoChetu

Maoni hayajaruhusiwa.