Vipi Khilafah itakabiliana na Umaskini wa ‘Kutengeneza’ -1

0

Tangu kuanguka kwa Khilafah mwaka 1924, wanadamu wamekuwa wakiishi kwa tabu sana chini ya mfumo wa ubepari, wachache sana ndio wamekuwa wakinufaika na mfumo huo. Kidunia umasikini wa kutengeneza umechukua nafasi kubwa katika matatizo ya wanadamu. Leo takriban watu billioni 2.3 wanaishi kwa dola moja (Tsh 2200), na billioni 3 wakiishi chini ya dola moja. Katika makundi hayo mawili, watu billion 1.3 hawana maji masafi na salama, billioni 3 hawana huduma ya umeme na billioni 1 wanaishi katika mazingira machafu.

Mwaka jana Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Oxfam Mark Goldring alisema ni kitu kisichokubalika kuona nusu ya masikini duniani wanamiliki kiasi kidogo sana cha rasilimali za dunia, huku mmoja kati ya watu tisa wanakwenda kulala na njaa, ilhali matajiri wamepata utajiri wao kupitia matumizi ya masikini.

Kwa mujibu wa taarifa za Oxfam za mwaka jana, watu wasiopungua 62 tu ndio wenye kumiliki kiasi kikubwa cha rasilimali duniani.  Aidha, Shirika la UNDP nalo liliwahi kutamka mwaka 1998 kuwa lau matajiri 255 wa dunia wakitoa kodi ya 4% kwenye utajiri wao, itatosha kutimiza mahitaji msingi ya watu wa ulimwengu wa tatu (developing countries.).

Umasikini wa kutengenezwa ndio umekuwa changamoto kubwa na chanzo cha matatizo mengi ulimwenguni. Kukithiri kwa riba, rushwa, wizi, ukahaba, utapeli, mauaji, ubakaji, kukosekana kwa mahitaji msingi ya mwanadamu nk. Huku tawala zinaonekana kutokuwa na masuluhisho ya kukabiliana na hali hiyo katika msingi wake, matokeo yake watawaliwa wengi wamekuwa ndani ya mashaka makubwa.

Kama ukitembelea magereza, vyumba vya kuhifadhia maiti na penginepo utakuta wahanga wengi wameathiriwa na umasikini huu wa kutengeneza. Kwa mfano, mfungwa ima kafungwa kwa kusingiziwa, au kama alikamatwa kwa wizi, mauaji, rushwa nk. Kimsingi ni mambo yaliosababishwa na umasikini wa kutengeneza. Tatizo la umasikini wa kutengenezwa pia ni chachu ya ushirikina kwani hufikia mahala mtu hukata tamaa ya kujikwamua ila kwa njia ya kishirikina inayopelekea kufanya mauaji ya watu wasio na hatia. Wimbi la mauaji ya maalbino na mauaji mengine yanadaiwa kuchochewa na imani za kishirikina kama mbinu ya kutafuta utajiri.

Ukiangalia ndani ya miamala kama ya kibiashara kumekuwa na udanganyifu mwingi sana, mpaka hufikia mahala muuza simu anakudanganya kuwa network ya simu yake inafanya kazi mpaka chini ya ardhi nk. Au biashara isiyokuwa hiyo utakuta kuna aina nyengine ya udanganyifu. Umasikini huu wa kutengeneza  ndio huwafanya watoto wadogo kulazimika kuacha shule na kukimbilia kufanya biashara ndogo ndogo na kazi mbali mbali ili kujikimu na kuwakimu wazazi wao.  Ukiangalia wimbi kubwa la watoto wa kike hukatishwa masomo yao kwa kushika mimba kutokana na tamaa za fedha na vitu, na mwishoe kuishia kwenye ukahaba ili kujikimu kimaisha. Leo idadi ya ndoa zinazovunjika zinaongezeka maradufu kwa usaliti au kukimbiwa kulikosababishwa na umasikini huu wa kutengeneza. Bila ya kutaja Idadi ya wanaojiuwa kuongezeka kila kukicha kwa sababu ya watu kushindwa kujikimu kimaisha. Umasikini huu wa kutengeneza umezua mashaka na taharuki kila pembe ya dunia, huku kikundi cha wachache hunufaika kupitia umasikini huu.

Kiislamu, umasikini ni hali ya kushindwa kujikimu kwa mahitaji msingi (mavazi, chakula, malazi). Hali hii ya umasikini kimsingi kuna upande wa matakwa ya Muumba, yaani qadhwaa ambayo ipo juu ya uwezo wa mwanadamu, wala si kwa sababu ya elimu, uduni wa fikra nk. Bali pia ni hali inayoweza kumtokea mwanadamu kama mtihani kwake. Mfano, kisa cha Nabii Ayoub (As) awali alikuwa na mali na watoto na akoondoshewa vyote katika kutahiniwa kwa kupewa maradhi kwa miaka kadhaa na baadae hali hio ikatoweka na kurudi katika hali yake ya mwanzo.

Kwa upande wa pili, kuna umasikini wa kutengeneza, huu haotokani na matakwa ya Muumba. Bali ni hali inayotekelezwa na mfumo wa ubepari kwa kushindwa kutatua matatizo ya watawaliwa, kuwanyonya rasilimali zao na kuwageuza kuwa watumishi na mitaji yao. Hali hii hutokana na uzembe, dhulma na uozo wa mfumo huo ikiwemo kuwabana raia, kubinafsisha rasilmali za Umma na kuwapa nguvu na uwezo wachache kumiliki kiasi kikubwa cha rasilimali hizo

 Haafiz Abdul-Karim

INAENDELEA………….

Leave A Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.